Institute of Languages (INSTL)
Permanent URI for this collection
Browse
Browsing Institute of Languages (INSTL) by Author "David, Majariwa"
Now showing 1 - 4 of 4
Results Per Page
Sort Options
Item Open Access Nafasi ya Leksikoni yenye Vipashio Ghairi kutoka Kiingereza na Kiarabu katika Fonolojia ya Leksikoni ya Kiswahili Sanifu(2023-03) David, MajariwaMakala haya yanahusu ubainishaji wa nafasi ya leksikoni ya mkopo yenye vipashio ghairi katika leksikoni ya Kiswahili sanifu. Data zilizotumiwa katika makala haya zilikusanywa kutoka makavazi ya Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mbinu za uhakiki matini na usomaji nyaraka zilitumiwa kukusanya data. Uhusiano wa matabaka ya leksikoni ya Kiswahili umeelezwa kwa kutumia modeli ya uhusiano wa KIINI-PEMBEZONI ya Itô na Mester (1995) sambamba na Nadharia ya Umbo Upeo (UU). Data imedhihirisha kuwa leksikoni ya Kiswahili inatoa ushahidi kuwa kuna matabaka mbalimbali ndani yake. Modeli iliyotumiwa imetuwezesha kubainisha mwingiliano taratibu na utabakishi wa leksikoni ya Kiswahili. Leksikoni ya Kiswahili yenye viambajengo ghairi husika imetambuliwa kisinkronia kwa kuwa viambajengo hivyo vina mchango katika sarufi ya Kiswahili (fonolojia ya leksikoni ya Kiswahili) hasa kuhusiana na mashartizuizi ya kimuundo. Matokeo yamebainisha kuwa mashartizuizi ya leksikoni ya Kiswahili iliyopokelewa kutoka Kiingereza na Kiarabu na viambajengo ghairi yanafanya kazi katika mawanda ya PEMBEZONI.Item Open Access Ukubalifu wa Silabi Funge katika Fonolojia ya Kiswahili(Mwanga wa Lugha, 2021) David, MajariwaMakala haya yanachunguza ukubalifu wa silabi funge katika fonolojia ya Kiswahili kwa kutumia mifano kutoka Kiarabu na Kiingereza. Tafiti kadhaa zilibainisha uchopezi wa irabu baada ya konsonanti funge kuwa ni mkakati wa urekebishaji unaotumiwa sana katika upokeaji wa maneno ya mkopo katika Kiswahili ili kuondoa silabi funge. Hata hivyo silabi funge zimebainika katika fonolojia ya Kiswahili. Kutokana na msingi kuwa mifumo ya fonolojia ya lugha hufikiriwa kuwa thabiti zaidi dhidi ya mabadiliko, kuna haja ya kuchunguza ukubalifu wa silabi funge hizo katika fonolojia ya Kiswahili. Data zilizotumika zilipatikana kutoka Kamusi ya Kiswahili Sanifu 2013 (KKS), Toleo la tatu. Nadharia ya Umbo Upeo sambamba na Nadharria ya fonolojia Amirifu zilitumiwa katika uchanganuzi wa data. Matokeo yanaonesha kuwa upangiliaji upya wa mashartizuizi unaeleza upenyezaji wa silabi funge katika Kiswahili na ukubalifu wa silabi funge hizo umeelezwa na fonolojia Amirifu. Uelekeo wa watumiaji wa lugha ya Kiswahili kutumia nguvu kwa uwekevu katika matumizi ya ala za matamshi umesababisha fonolojia ya Kiswahili kuzuia uchopezi wa irabu katika upokeaji wa maneno yenye silabi funge kutoka Kiingereza na Kiarabu.Item Open Access Upenyezaji na Ukubalifu wa Mkururo wa Konsonanti katika Fonolojia ya Kiswahili: Mifano katika Maneno Yaliyopokelewa kutoka Kiingereza na Kiarabu(Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, 2021) David, MajariwaMakala haya yanachunguza jinsi mikururo ya konsonanti [Skr-]/[Sk-], [Spr-]/[Sp-], na [Str-]/[St-] ilivyopokelewa katika fonolojia ya Kiswahili kutoka Kiarabu na Kiingereza. Lengo kuu ni kuelezea jinsi mikururo hiyo ya konsonanti ilivyopenyeza na kukubalika katika mfumo wa fonolojia ya Kiswahili. Mifumo ya fonolojia ya lugha inafikiriwa kuwa thabiti zaidi dhidi ya mabadiliko ikilinganishwa na nyanja nyingine za isimu. Data zilizotumika zilipatikana kutoka Kamusi ya Kiswahili Sanifu (KKS) (2013), Toleo la Tatu pamoja na Bosha (1993). Mbinu ya orodhahakiki na usomaji nyaraka zilitumiwa kupata data. Nadharia ya Umbo Upeo ilitumiwa katika uchanganuzi wa data. Uchopezi wa irabu ni mkakati unaozingatiwa sana wakati wa urekebishaji wa mkururo wa konsonanti katika maneno yanayopokelewa katika Kiswahili (Mwita, 2014; Akidah, 2013). Hata hivyo, imebainika kuwa mikururo wa konsonanti [Skr-]/[Sk-], [Spr-]/[Sp-], na [Str-]/[St-] ilighairi mikakati ya urekebishaji na kupenyeza katika fonolojia ya Kiswahili. Upokeaji wa mikururo hiyo ya konsonanti uliwezekana kupitia upangiliaji upya wa mashartizuizi ya Kiswahili. Upangiliaji wa mashartizuizi ulichochewa na haja ya kuwa na uwekevu wa nguvu katika utamkaji. Hivyo, ukubalifu wa mikururo ya konsonanti umeelezwa kupita wepesi wa utamkaji uliochochea upangiliaji wa mashartizuizi ya mfuatano wa konsonanti katika Kiswahili.Item Open Access Upokeaji na Ukubalifu wa Vitamkwa vya Kiarabu na Kiingereza katika Fonolojia ya Kiswahili(Jarida la Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, 2021) David, MajariwaMakala hii inachunguza jinsi vitamkwa vya kigeni [χ], [ɣ], [ð] na [θ] vilivyopokelewa katika fonolojia ya Kiswahili kutoka Kiarabu na Kiingereza. Lengo la makala hii ni kuelezea sababu za ukubalifu2 wa vitamkwa hivyo katika mfumo wa fonolojia ya Kiswahili, licha ya mifumo ya fonolojia ya lugha kufikiriwa kuwa thabiti zaidi dhidi ya mabadiliko. Data zilizotumika zilipatikana kutoka Kamusi ya Kiswahili Sanifu (KKS) (2013) Toleo la Tatu na Bosha (1993). Nadharia ya Umbo Upeo imetumika katika uchanganuzi wa data za makala hii. Kuna mikakati ya urekebishaji kadhaa ambayo inaelezea jinsi vitamkwa vinavyoshughulikiwa katika upokeaji wa maneno ya mkopo katika muktadha wa nadharia hii. Hata hivyo, ilibainika kuwa vitamkwa vya kigeni [χ], [ɣ], [ð] na [θ] vilighairi mikakati hiyo ya urekebishaji na kupenyeza katika fonolojia ya Kiswahili. Upokeaji wa vitamkwa hivyo uliwezekana kupitia upangiliaji upya wa mashartizuizi ya Kiswahili katika Umbo Upeo. Vitamkwa vilivyopokelewa vilikubalika katika mfumo wa orodha ya konsonanti za Kiswahili kwa kuzingatia msingi wa iktisadi ya sifa na mvutano pande mbili. Vitamkwa hivyo vilipokelewa kutokana na kuwapo kwa mapengo ya vitamkwa hivyo katika orodha ya vitamkwa vya Kiswahili.